Tuesday, August 22, 2017

SIMULIZI: JAMANI MCHUNGAJI!!


Image result for jamani mchungaji

Masikio yake hayakuamini anachokisikia lakini ubongo wake uliamini kuwa mkewe alikuwa kwenye ndoto nzito sana, jasho lilikuwa linamtoka na alikuwa anajiviringisha pale kitandani kwa staili za ajabu ajabu
"Mchungaji.,ah! mchungaji...mchungaji" ndizo sauti alizokuwa anatoa mwanamke huyu
"Mh! ndoto gani tena hizi jamani au ndio....," alisita kumalizia neno hilo kwani kwa misingi yake ya dini ilikuwa haipaswi kumuhukumu mwanadamu mwenzako bila kumshrikisha Mungu muumba wa vyote. Miguno hiyo ilikuwa inashabihiana kabisa na ile ambayo huwa inasikika katika filamu za ngono.
Alitua ‘briefcase’ yake chini na kulegeza tai yake kabla ya kuondoa koti lake la suti, tayari ilikuwa saa nne usiku akiwa ametoka kwenye kikao cha kampuni. miguno iliyoendelea pale kitandani ilimtia hasira kiasi fulani lakini jina lililotajwa ndio lilimkera zaidi
"Honey! honey, iam back" taratibu akamwamsha na kuikatisha ndoto yake.
"Mh! mchungaji ah! mume wangu, umerudi karibu, saa ngapi hivi" kwa sauti ya ulevi wa usingizi alianza kuzungumza yule mwanamke huku akiyapikicha macho yake kwa kutumia kiganja kimoja na mkono mwingine ukiishikilia kanga iliyokuwa inataka kudondoka kutoka kifuani, mwanga wa taa iliyokuwa imewashwa ilimsumbua kuizoea hali.
Hasira ilimkaba kooni kijana huyu, alijaribu kutabasamu lakini sura yake ilifanana na mtu aliyepokea barua ya kufukuzwa kazi huku nyumbani akiwa na familia kubwa pamoja na wakwe waliokuja kuchukua mahari yao ambayo ilikuwa haijamaliziwa bado. Alichukizwa sana na suala la mke wake kukosea jina lake na kumuita mchungaji, mwanzoni alilisikia hilo jina katika ndoto lakini sasa alikuwa anamsikia mkewe akilitaja jina hilo wakati ameyafumbua macho yake.
* * * *
Lilikuwa suala gumu sana kumshawishi kijana Timoth aweze kukuelewa kuhusu umuhimu wa kuwa na mwenza ndani ya nyumba. Shughuli za kufua, kuosha vyombo na kufanya usafi ndani ya nyumba yake zilimchosha sana lakini hakutaka mke.
Aliyaogopa mapenzi sana kupindukia visa vya mafumanizi alivyovisoma kwenye magazeti na kusikia redioni vilimtikisa sana kaka huyu aliyekuwa na miaka takribani ishirini na tisa (29) na tayari akiwa na mafanikio yake kama kijana kwa mshahara alioupata kutokana na kazi yake ya afisa masoko wa kampuni ya usafirishaji ya Lookman ya jijini Dar-es-salaam.
Kwa ushauri wa mama yake mzazi na pia mchungaji wa kanisa lake bwana Marko, Timoth alianza kufikiria kuhusu suala hilo na hatimaye hisia za mapenzi alizokuwa amezifungia gerezani akazipa msamaha zikawa huru na uhuru huo zikautumia kumwangukia binti mrembo mwimba kwaya hapo kanisani aliyeitwa Noela, halikuwa suala gumu sana kwani wachungaji walikuwa kati yake hvyo Noela hakuleta longolongo uhusiano ukaanza rasmi hadi walipofunga ndoa takatifu kanisani hapo. Japo alikuwa anahofu ya kutendwa lakini aliifunga akili yake na kusema maneno haya.
“Nipo tayari kumuoa binti Noela Philemon, na nitaishi naye katika shida na raha hadi hapo kifo kitakapotutenganisha” makofi, nderemo na vifijo vilifuatia.
Timoth Getafe na Noela Philemon wakawa mke na mume rasmi!!
Timoth aliamini alikuwa amekosa mengi kwa kuwa katika maisha ya ukapera muda wote ule, kwani raha alizozipata kwa kuwa na Noela kama mke wake alijihisi yupo nchi ya kufikirika ambayo ni zaidi ya jengo la kifalme huko uingereza, zaidi ya Tanzania na amani yake, zaidi ya raha anazopata mtoto kwa kunyonya ziwa la mama huku joto la asili lillojaa upendo wa kweli wa mama likipenya katika ngozi yake.
Noela alikuwa akimpa Timoth heshima zote za kuwa mume. Alimuheshimu na kumjali sana kama mtoto wake. Alimdekeza na kumjali, Timoth akajihisi kama yupo mikononi mwa bi. Mariam ambaye ni mama yake mzazi. Taratibu akausahau msiba uliotokea mwezi mmoja uliopita, kifo cha baba yake mzazi kwa ajali ya gari.
"Mh! nisingekubaliana na mchungaji na mama haya ningeyapata wapi?" alijiuliza Tim siku moja akiwa anakula chakula kizuri cha mkewe huku glasi kubwa ya juisi iliyokuwa inatoa jasho jasho za ubaridi ikimtazama.
Wakati wote huo Noela alikuwa mama wa nyumbani hakuwa na ajira bado zaidi ya kuimba kwaya kanisani shughuli ambayo haikuwa na kipato chochote kwani ilikuwa ni ya kujitolea kwa dhumuni la kumtumikia Mungu.
Noela alikuwa na miaka saba katika mstari wa mbele wa kwaya hiyo.
"Mpenzi samahani kama nitakuwa naingilia mipango yako....nataka kuomba kitu" Noela alimwambia mumewe miezi miwili wakiwa ndoani, wakati huo alikuwa akimpapasa papasa mumewe kifuani.
"Sema tu malaika wangu usiogope ni wewe Mungu amenipangia" Timoth alimwondoa hofu mkewe huku na yeye akimsukasuka nywele zake pasi na ujuzi wowote.
"Asante mume wangu mi nilikuwa nataka hapa nyumbani japo nipate kitu cha kuniweka bize na mi sio kingine zaidi ya ufugaji mdogo mdogo, si unajua ninavyopenda kufuga mie" alijieleza Noela huku akijiumauma midomo yake. Hakuweza kumuangalia machoni mume wake.
"Hapa nina mke kweli, yaani hilo sio ombi mke wangu il-hali umependa mwenyewe, nitakutimizia" alijibu kwa furaha Timoth huku akiendelea kuchezea nywele za mkewe.
Kama alivyoahidiwa ni kweli kwa haraka mabanda yalijengwa Noela akaanza kufuga kuku, kanga na bata baadae Mbuzi na hatimaye n'gombe, kwa kweli alikuwa mwanamke mchapakazi sana na alistahili pongezi zote.
* * * * *
Zoezi la kwenda nchini Uganda kurekodi mkanda wa video katika kwaya ya kanisa lao lilimlazimu Noela kutafuta kwa haraka kijana ambaye atahudumia mifugo yake kwa hizo wiki mbili ambazo hatakuwepo pale nyumbani. Timothy asingeweza kuwahudumia mifugo kwa wakati, kazi zake zilikuwa hazitabiriki. Kwa kusaidiana na mume wake walijitahidi kwa uwezo wao wote pamoja na kusaidiana na wapendwa wengine wa kanisa kumtafuta kijana wa kazi.
* * * *
Oscar Simon alikuwa kijana kutoka Kigoma ambaye ndio alipata fursa hiyo ya kuwahudumia viumbe wale.
Kijana huyu wa kabila la Kiha kutokana na kazi ngumu za kusukuma mikokoteni na ubebaji wa mizigo (Kuli) zilikitawanyisha kifua chake katika pande mbili zilizojaa haswa. Urefu aliobarikiwa tofauti na Waha wengi walivyokuwa wafupi ulimfanya awe na mwonekano wa kipekee sana na kuonekana mwanaume wa shoka, weusi wake na tabu nyingi alizopitia ziliuficha utanashati wake kabisa. Kazi ya muda mfupi aliyoipata kwa Noela ilikuwa kati ya kazi nyepesi alizowahi kupitia.
Ilikuwa kama bahati, baada ya kuwa amegonga mageti mengi sana kuomba ajira jijini Dar es salaam. Hatimaye bahati yake ikawa pia bahati kwa familia hii ya Noela na Timoth maeneo ya Kinondoni Studio jijini hapo ambayo hakika ilikuwa inamuhitaji kwa wakati huo.
Timothy akawa ameipata ajira!!
* * * * *
Picha ya ajabu ilianza kumjia Noela akiwa kwenye basi pamoja na wanakwaya wenzake. Aliona inajijenga picha ya mwanaume mbele yake, sura haikuwa ngeni sana machoni pake,mwanaume yule alizidi kupiga hatua kumfuata, kadri alivyokuwa anasogea na yeye (Noela) alizidi kutamani amfikie, alikuwa amevaa vesti nyeupe na pensi fupi ambayo ilikuwa imechakaa yeye (Noela) alikuwa amevaa kitop pamoja na skin tight, mazingra yale yalikuwa kama ufukweni lakini palikuwa na kitanda kilichokuwa na godoro tayari, taratibu Noela alijilaza chali kitandani akiwa na mategemeo kuwa na yule kijana atajilaza pale, mara akaanza kurudi kinyumenyume kwa hofu yule kijana, matamanio ya Noela yalikuwa juu alianza kumbembeleza yule kijana lakini ni kama alipatwa na hofu ya ghafla hvyo hakuweza kumsogelea Noela.
"Njoo haraka nasema!!" alipiga kelele Noela na kushtushwa na vicheko vya wanakwaya wenzake ndani ya gari.
"Aah! kumbe anaota kanishtua kweli loh!" mwanakwaya aliyekuwa pembeni ya Noela alisema huku akishndwa kujizuia kucheka. Noela alikuwa amepiga kelele sana bila kujua kama amefanya hivyo
Aibu aibu zikamkumba Noela na kujipikicha macho yake ni kweli ilikuwa ndoto lakini ndoto gani hiyo jamani!!!! alijiuliza Noela kimoyomoyo huku safari ikiendelea. Hakutaka kulala tena akachukua kitabu chake cha nyimbo za mapambio akaanza kumuimbia Mungu kwa sauti ya chini, mashairi yake yakamvutia aliyekuwa pembeni yake na yeye akaanza kuimba, na waliokuwa pembeni wakafuatisha hatimaye wakaunganisha sauti zao, Noela akapandisha sauti yake akaongoza mashairi, kicheko kikasahaulika kila mtu akawa ametekwa na wimbo huo.
Safari ikaendelea, likawa suala la bandika bandua!!!!
Hadi wanaifikia boda ya Namanga kuingia nchini Kenya bado nyimbo ziliendelea kulindima.
Ukaguzi wa hati za kusafiria ndio ulikatisha burudani yao.
Wote wakawa kimya kwa muda!!!
****
"Karibu mke wangu mpenzi jamani nimekumis namshukuru Mungu umerudi salama na kazi mliyoifanya imebarikiwa katika bwana" Timoth alimlaki mkewe kwa maneno hayo mazuri huku akimkumbatia siku aliyokuwa amerejea baada ya kuwa mbali na nyumba yake kwa siku nyingi.
"Asante mume wangu tunamshukuru Mungu kwa yote aliyotutendea katika safari yetu" alijibu kwa furaha Noela.
"Shkamoo mama!" ilitoka salamu nyuma ya Noela.
"Marah...." alisita kuitikia Noela baada ya kugundua aliyekuwa anamsalimia, macho yalimtoka hadi yule kijana akapata hofu, alikuwa ni Oscar kijana aliyekuwa amepewa ajira kwa muda kuhudumia mifugo pale nyumbani.
"We ndio nani...ah! ni Oscar ah? marahaba" alianza kujiumauma Noela na dhahiri alionyesha mshtuko mkubwa.
"Vipi mke wangu kwani.." alihoji Timoth bila kumaanisha sana.
"Ah! ah! mh? hamna kitu wala" hofu ilizidi kumwingia.
Hofu na uoga alioupata mkewe (Noela), Timoth alitambua mara moja, hakuijua sababu hasa na hakutaka kumuuliza mbele ya Oscar kijana mlisha mifugo kwa muda.
"Kwa hiyo Oscar aondoke lini mke wangu naona mwenye mifugo mwenyewe ndo umefika" Timoth alimuuliza mkewe wakati ametoka bafuni akijiremba kidogo mbele ya dressing table,
"Vipi utendaji wake ni mzuri?" alihoji Noela
"Mh! Sijawahi kupata malalamiko kutoka kwa kuku wala mbuzi yeyote nadhani kila kitu kinaenda vizuri" alitania Timoth huku akimtekenya mkewe ambaye aliruka juu taulo ikaanguka chini, kwa aibu aibu akajiziba kifua chake lakini akakiachia tena alivyokumbuka yule ni mumewe.
"Honey kabla hatujalala ni kwamba kanisa limetoa punguzo la bei za ng’ombe kwa waumini wake, naomba kama inawezekana na sisi tuanze kufuga n'gombe, eneo letu ni kubwa linaruhusu" kwa sauti ya kunon'goneza huku akipapasa kifua cha mumewe Noela alizungumza.
"Mke wangu wewe ndo mwenye maamuzi kwenye mifugu, tutanunua hao n'gombe, basi itabidi Oscar abaki kidogo ili aweze kukusaidia au unasemaje?"
"Haina neno mume wangu, nafurahi kuwa mkeo" alijibu Noela.
Usiku wa siku hiyo ulikuwa mrefu sana kwa Noela alitamani pakuche ili apate fursa ya kuhakikisha ndoto yake ya ndani ya gari akiwa safarini kama ina ukweli wowote
"Hivi yawezekana nimemwota huyo kijana? Mbona wanafanana sana jamani dah!, lakini mbona siku ya kwanza nilimuona wa kawaida tu, tena sana" Noela alijiuliza wakati anagalagala kitandani kutafuta usingizi ambao tayari ulishampitia mume wake mapema kabisa.
Hatimaye usingizi ulimpitia na asubuhi ikafika.
"Mpenzi amka maji ya kuoga tayari, yatapoa na hii baridi utakoma" Noela alimwamsha mumewe kwa sauti ya upole na mahaba tele.
Bila kuhoji chochote alikurupuka pale kitandani akachukua taulo akajifunga akambussu mkewe shavuni kisha akaingia bafuni.
"Haya kwa heri mume wangu na kazi njema" Noela alimuaga Timoth baada ya kuwa amevaa nguo na kupata kifungua kinywa.
"Asante mama yangu na wewe ubaki salama na Mungu awalinde" alijibu Timoth huku akirekebisha tai yake, Noela akamsogelea akamsaidia kuirekebisha ile tai kisha akambusu katika papi za mdomo wake, Timoth akatoa tabasamu la nguvu akampiga kibao cha kimapenzi katika shavu lake lililokuwa linatangaza vishimo vidogo pande zote. Kisha akafungua mlango na kutoweka.
Noela akabaki kumsindikiza kwa macho hadi alipoishia.
ITAENDELEA

Related Posts

SIMULIZI: JAMANI MCHUNGAJI!!
4/ 5
Oleh